Header Ads

UBATIZO

Kwanini nibatizwe? Ubatizo upi ni sahihi kibilia?. Ni wakati upi na nani anatakiwa kubatizwa? Je, ni kabla ya kupokea wokovu au baada? Faida zake ni zipi? .

Kwanza kabisa; kuna batizo zitokazo kwa wanadamu na pia upo ubatizo unaotoka kwa Mungu. Tunajua hili kutokana na Yesu alipowauliza makuhani na wazee wa Israel kwa Kusema “Nitawauliza neno moja, nanyi mnijibu, kisha nitawaambia ni kwa mamlaka gani nayatenda haya. Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni” (Mk.11:30-32).

Kutoka hapo tunajuwa kumbe ubatizo ule wa Yohana ulitoka Mbinguni. Pia kabla ya Yohana Mbatizaji, kulikuwa na aina mbalimbali za batizo ambazo hazikuwa kama ubatizo wa yohana. Hii ni kutokana na swali ambalo watu kadhaa waliulizwa na mtume Paulo kwa kusema “Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana” (matendo,19:3). Hivyo kutoka hapo pia tunajua kumbe hata wakati wa mitume kulikuwa na batizo aina mbalimbali zilizoletwa na wanadamu
Kabla Yesu hajaondoka duniani, naye alikuwa anabatiza watu kupitia wanafunzi wake. Na aina ya Ubatizo aliokuwa anautumia ulikuwa ni ule uliotoka Mbinguni ulioletwa kwa mkono wa Yohana. Kama ilivyoandikwa “Baada ya hayo Yesu na wanafunzi wake walikwenda mpaka nchi ya Uyahudi; akashinda huko pamoja nao, akabatiza” (yoh.3:22,10:40). Na huu ndiyo ubatizo sahihi kibibilia ambao Yesu aliowaachia wanafunzi wake mpaka leo.

Sasa Ubatizo wa Maji Mengi huu wa Yohana Mbatizaji Mungu ameuweka ili kwa Njia hiyo nawewe ushiriki kifo cha Yesu kwa kufa pamoja naye na kufufuka pamoja naye kwa njia ya kuzamishwa na kuinuliwa katika maji. Kama ilivyoandikwa “sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake” na tena “tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima”. na tena “Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye” (Rum.6:3-6, Col.2:12). Hivyo tunaona kumbe unapobatizwa, mambo halisi hufanyika wala sio ishara tu.

Siku unayo-batizwa kwa maji mengi ndiyo siku ambayo 1) unakufa pamoja na Kristo msalabani. 2) unafufuka pamoja na Yesu mautini. 3). Unapokea Uwezo wa kuenenda katika hali ya “upya wa uzima” alionao Yesu sasa. 4) unakuwa umetimiza haki yote. Maana imeandikwa “mshahara wa dhambi ni mauti”. Na kwasabu wewe hapo mwanzo ulikuwa mdhambi… Unahukumiwa mauti pamoja na Yesu kwa njia ya msalaba na mauti yake. Hivyo hutahukumiwa mauti ile siku ya kuuhukumu ulimwengu wote (yohana.5:24)

Tunajuwa kuwa Yesu aliposulubiwa msalabani hakufa muda uleule; bali alisulubiwa saa tatu lakini akafa saa tisa (Mk. 15:24,34). Vivyohivyo Kuokoka maana Yake ni kuzaliwa mala ya pili kunako ambatana na kupokea utakaso wa dhambi zote na kunyweshwa ua kumpokea Roho Mtakatifu ndani yako aishi nawe milele. Na kwasababu hiyo wewe unakuwa kiumbe Kipya uliye Mwana wa Mungu, uliye mtakatifu na uzima wa Milele unakuwa ndani yako. Kama ilivyoandikwa “alituokoa;…, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa mara ya pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu”, na tena “Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima “(tito.3:4-7, 1yoh.5:12).

Kwahiyo mtu huyu alie-okoka anakuwa amezaliwa mara ya pili na amesulubiwa msalabani pasipo kuzikwa utu wake wa kale na kufufuka pamoja na Yesu. Kama ilivyoandikwa “hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake” (gal.5:24). Hivyo utu wake wa kale unakuwa bado haujazikwa, kwasababu utu wa kale huzikwa katika ubatizo wa maji mengi.Kwahiyo kama hujabatizwa atakuwa kwenye vita kali daima kati ya roho yako na mwili wako mpaka pale atakapouzika huo utu wako katika ubatizo.

Hivyo haijalishi wewe umeokoka miaka mingi kiasi gani. Lakini pasipo ubatizo wa maji Mengi bado haujakamilika. Hauja-itimiza haki yote. Kwani kumbukumbu za wewe kufa na kufufuka pamoja na Kristo hazipo mbele za Mungu mpaka utakapo kubali kubatizwa kwa ubatizo wa Maji mengi. Usitegemee ubatizo wa kunyunyizia kichwani kwani kwa huo haiwezekani kushiriki mauti na ufufuo wa Yesu Kristo. Kama inavyosema “Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye”.

Siku unayobatizwa ndiyo siku unayozika utu wako wa kale na kuhukumiwa mauti pamoja na Yesu msalabani ili siku ile ya hukumu usije ukahukumiwa mauti kama wengine ambao wao watahukumiwa mauti. Maana imeandikwa “tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote” (2Kor.5:14). Kwahiyo huo ubatizo wa Kuzamishwa kwenye maji ni ili uunganishwe na Yesu katika mauti na uzima wake. Ukibatizwa unafanya “final separation from the world”.
Mtu anatakiwa kubatizwa baada ya kupokea wokovu kwanza na sio kabla ya kuamini (Mk.16:16). Maana sababu nyingine ya kubatizwa ni matokeo ya utii yathibitishayo kuwa dhamiri zako zimefanywa upya. Kama ilivyoandikwa “ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; .., jibu la dhamiri safi mbele za Mungu, kwa kufufuka kwake Yesu Kristo” (1pet.3:21). Sasa jibu la dhamiri haliwezi kuwepo kwa mtoto mchanga kimwili, kwasababu mtu anapo-okoka (born again) ndipo anatakaswa dhamiri zake na kuanza kuzichukia dhambi alizokuwa anazitenda kabla, na roho yake huanza kuumia akiziona dhambi (ebr.9:14, 2pet.2:8)

“utashiriki vipi mauti ya Mwanangu Yesu kwa kunyunyiziwa maji kichwani? Niambie, Je, kwa kunyunyiziwa maji utatimizaje neno langu lisemalo “Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye”?. “kama vile ambavyo haikuwezekana Mwanangu afe bila kwenda ndani ya nchi chini; vivyohivyo nawewe haiwezekani kushiriki mauti ya Mwanangu pasipo kwenda ndani ya maji”. kwa kubatizwa Yesu ndani ya maji, akatia mhuri na kutangaza mauti na ufufuo wake jinsi utakavyokuwa. Hivyo nawewe imekupasa kuenenda kwa jinsi hiyohiyo.
Laana na magonjwa ya kurithi hukaa na hupata kibali kutokana na wewe kuwa na utu wa kale. Lakini unapobatizwa hayo yote huzikwa na hayawi na mamlaka tena kwani unakuwa “katika upya wa uzima” (rum.6:4). Baada ya kuokoka nilikuwa nabisha sana. Hadi Mungu mwenyewe aliposema na mimi. Na baaada ya kufunuliwa tu bila kuchelewa nilienda nikabatizwa kwa maji mengi. Hivyo hata wewe unaweza ukaenda ukabatizwa bila kuhama hilo dhehebu lako. Nenda Kabatizwe usifungwe na udhehebu ukakosa ufalme.

Sio dhambi, na sio ukosefu wa imani kuamua kubatizwa kwa mala nyingine kama ukigundua ubatizo wa kwanza huakuwa kama neno linavyotaka. Hata mimi nilitumia hoja kama hiyo kukataa kubatizwa kwa maji mengi kwa kusema “nilibatizwa tayari tangu mtoto”. Lakini Bwana akasema “mbona kwenye Matendo 19:2-5 mtume Paulo aliwabatiza mala ya pili watu kadhaa waliokuwa wamebatizwa na yohana mbatizaji?”.

Hautakiwi kubatizwa kama hujapokea wokovu kwanza. Kibiblia mtu haokoki kwa kubatizwa kwa maji. Unapokea wokovu kwanza ndipo unaenda kubatizwa. Mtu asikudanganye kwa kusema siku unayobatizwa ndiyo unayozaliwa mala ya pili- Huo ni uongo. Ukibatizwa kabla ya wokovu ni sawa na mtu anae-oga tu.

Kama kweli wewe ni mteule wa Mungu; Jambo hili la ubatizo hutakuwa na amani nalo mpaka utakapokubali na kutii kwa kwenda kubatizwa. Ndipo moyo wako utakapotulia. Maana Mungu hawezi kumtumia mtu “to the full” kama bado hujabatizwa. Yesu anasema “Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu”(Yohana.3:5). AMINA.
Mwandishi: NZUNDA Ibrahim (0754 210 627)

Hakuna maoni

Inaendeshwa na Blogger.